JAMANI mu hali gani, najua mko poa, yangu hali bulibuli, nami ni miongoni mwa watu waliopendelewa na Mwenyezi Mungu kuendelea kuvuta pumzi yake huku nikitabasamu na kuonesha meno yangu mawili ya dhahabu.
Wenye kisokolo kwinyu utawasikia ninajishaua, jamani ungelionaje jino langu la dhahabu bila kutabasamu? Ungekuwa utunda hapo ungesema kwa vile umefichwa na nguo zaidi ya tatu na anayetakiwa kuuona ni laazizi wako, japo siku hizi umekuwa kama mkufu unaonekana hadharani.
Siku hizi viuno vimegeuka kama shingo utunda nje, loh! Huolewi unasema umerogwa kumbe mchawi ni wewe usiyejua mwanaume anataka nini.
Jamani kama ni siri ya mpishi jungu halifunuliwi mpaka mlaji afungue mwenyewe na kuyakuta maanjumati ndani. Kwa vile hakuviona awali lazima awe na hamu navyo na akila lazima avione vitamu. Lakini siku hizi wanawake sehemu za siri si siri tena, zinaonekana ovyo kama muuza samaki aliyewaanika kwenye sinia.
Jamani nimeanza kama nimekatwa kichwa kutokana na tabia zenu zinazonitia kichefuchefu, kwani mkivaa nguo za heshima hampendezi? Hebu tubadilike jamani mwanaume siyo kama tetele mpaka umpe mtama mwingi ndiyo umkamate.
Kujiheshimu kunakuongezea maksi, hata mwanaume atakayekuja kwako atajua huyu ni wanamke wa kukaa ndani na si wa kukutumia kama chombo cha starehe.
Ehe! Nimekumbuka kitu kimoja ndicho hasa kilichonifanya niweke makalio chini nielezee hili, jamani mwanamke anatafutwa lakini ndoa anaitengeneza mwenyewe.
Umenipata? Au nimekuacha unatapatapa, unajua sababu ya uchumba kuchukua muda mrefu au kuvunjika kabla ya ndoa?
Siku zote mwanaume akimuona mwanamke huvutiwa naye hivyo huanza taratibu za kumvuta kwake. Baada ya kuelewana hapo mipango ya uchumba huanza na hatimaye mahari kisha ndoa kamili. Lakini wengi wamekuwa wakipata bahati ya kuchumbiwa lakini wanaachwa njiani.
Mnajua ni kwa nini? Basi tega sikio usijesema hukusikia. Jamani uchumba siyo ndoa, ukichumbiwa unakuwa chini ya uangalizi wa kuonekana kama kweli tabia zako zinafaa kuwa mke wa kufa na kuzikana au chombo cha starehe.
Lakini wengi wamekuwa na dharau na kiburi kwa wachumba wao hata kudiriki kusema, kuolewa siyo lazima wana uamuzi wa kuoa au kuacha pengine alichelewa kupokea simu au siku hiyo hakwenda kwa sababu fulani. Si hao tu wapo wanaogeuza uchumba mtaji kutaka kupata vitu vya gharama kwa wachumba wao na wakivikosa hutishia kuvunja uchumba.
Shutuuuuu! Jamani unatishia ushuzi wakati una tumbo la kuendesha utajichafua, wengi huchoshwa na tabia za wapenzi wao ambao hujionesha tabia zao za kijinga hata kabla ya ndoa, nani anakubali kuingiza bomu ndani akijua litapasuka wakati wowote kwa tabia zako.
Huna aibu wala heshima, unaringia umbile na sura na kusahau tabia ndiyo silaha kubwa katika maisha ya ndoa. Nina imani nimesomeka kwa leo haya machache yanatosha.
credit with: GlobalPublishers
No comments: