» » MKE ANAYEDAIWA KUPANGA KUMUUA MUMEWE KORTINI


038 b2c8f

MWANAMKE anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa ndoa na mtoto wa mume huyo, amepandishwa mahakamani akiwa na mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo. (HM)
Janeth Jackson (32), mkazi wa Moshono, Arusha na Novatus Elias, walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora, wakisomewa makosa mawili ya kula njama ya kutaka kumuua Simon Jackson ambaye ndiye mume wa Janeth.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Edna Kasala, alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote walitenda kosa la pili la kula njama na kutaka kumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa mke mwingine kwa mume huyo anayeishi Bukoba, mkoani Kagera.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kasala iliomba mahakama kuwanyima dhamana washtakiwa, kwa sababu watuhumiwa wengine wawili wanatafutwa hivyo na upelelezi haujakamilika.
Alidai kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi hayo ya kuwanyima dhamana washtakiwa yameambatana na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.
“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya washtakiwa kikatiba, lakini kutokana na mazingira ya kesi hii kuwa magumu, tunaomba dhamana isitolewe ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa kesi hii,” alidai Kasala.
Kwa upande wake,Wakili wa utetezi, Fidelis Peter, alipinga maombi hayo na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na kwamba hilo ni kosa lao la kwanza.
Sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa mashtaka, ni kwamba washtakiwa wanaweza kuvuruga upepelezi wakiachiwa siyo za msingi kwani ni watu wanaoaminika katika jamii.
“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana washtakiwa hazina uzito wowote, pia mshtakiwa wa kwanza (Janeth) ana mtoto wa miezi sita na tangu akamatwe alhamisi iliyopita hajamwona wala kumnyonyesha hivyo anastahili kupewa dhamana,”alidai Wakili Peter.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, Hakimu Kamuzora, alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kuamuru watuhumiwa wapelekwe mahabusu hadi Agosti 5, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi jijini hapa, inadaiwa Janeth alitaka kumuua mumewe ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na mwanaye wa kiume, ili arithi mali na utajiri alionao mfanyabiashara huyo. 

Chanzo: mwananchi

Tunaomba Maoni yako Hapa :

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply