» » WALINZI WA AMANI DARFUR WADAIWA HAWANA ZANA ZA KISASA


030 d4b74
KATIBU Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim, amesema umahiri wa vikosi vya kulinda amani Darfur na kwingine Afrika unatia shaka, kwani vinakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi ikiwamo zana za kisasa. (HM)
Kauli ya Dk Salim inakuja ikiwa ni siku chache baada ya kuuawa kwa wanajeshi saba wa Tanzania waliokuwa wakitumikia Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa na Afrika (Unamid).
Wanajeshi hao waliuawa wakiwa katika majukumu yao na kundi la Wanamgambo, linalodaiwa kuiunga mkono Serikali ya Rais Said al-Bashar la Janjaweed.
Dk Salim alisema himizo la kutaka kubadilishwa kwa kifungu cha sita kwenda saba, liende sanjari na zana za kisasa ambazo waasi hao wanatumia ikilinganishwa na walinzi wa amani wanaotumia silaha za kawaida.
“Nakumbuka wakati fulani nikiwa Mjumbe wa Umoja wa Afrika, nilikosa hata helikopta kusafirisha vikosi,” alisema na Dk Salim na kuongeza:
“Darfur utulivu haupo maana eneo hilo linakabiliwa na makundi mengi ya wanamgambo… kuna wanaojiita wanaukombozi, kuna hawa Janjaweed na pia kuna vikosi vya Serikali ya Sudan, makundi yote haya yanakuonyesha jinsi eneo hili lisivyo salama.”
Dk Salim alikuwa akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusiana na mauaji ya wanajeshi saba wa Tanzania.
“Vikosi vya Unamid kwa sasa havina uwezo wa kukabiliana na nguvu za makundi ya wanamgambo,” alisema Dk Salimu na kuongeza:
“Haya makundi yana silaha nzito na kisasa ikilinganisha na silaha ndogo ambazo hazifanani na waasi, zaidi ya hapo hawa walinzi wa amani hawaruhusiwi kutumia nguvu.”
Juzi, wakati akiaga miili ya wapiganaji hao, Rais Jakaya Kikwete, alielezea kukerwa, kuumizwa na kukasirishwa na mauaji ya askari hao ambao kazi yao ni kulinda amani ambayo ikipatikana itakuwa neema kwa Wasudan.
Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alitaka UN kubadilisha muundo wa vifungu hivyo.

News via: mwananchi

Tunaomba Maoni yako Hapa :

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply