» » » Sumaye: ' Watanzania tuepukane na Ubinafsi kama tunahitaji Mafanikio'

Dar es Salaam: Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amewataka Watanzania kuacha ubinafsi na kujitolea kwa jamii katika kukabiliana na majanga ya njaa, mazingira, maji na elimu ambayo yamekuwa ni chanzo cha pengo kati ya tabaka la matajiri na masikini nchini.

Sumaye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya kwa Wanajumuiya wa Chama cha Maendeleo kwa wilaya za Bonde la Ufa (Norivada), alisema umoja ndiyo nguzo pekee itakayowaondoa Watanzania kwenye umasikini.


Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye.

"Ubinafsi umekuwa janga, leo hii wapo baadhi ya Watanzania wana ubinafsi wa hali ya juu na kujijali wao na familia zao bila kujali wengine, ambao hawapati hata moja ya kumi ya kile wanachopata wao.

"Nawaomba epukeni tabia ya ubinafsi, kama mnahitaji mafanikio, basi washirikisheni na wengine katika yale ambayo tunayataka kwenye familia zetu, ikiwamo kuwasaidia kupata elimu bora, afya na kukabiliana na majanga mengine kama ya njaa," alisema Sumaye.

Mwenyekiti wa Norivida Taifa, Joseph Tango alisema jumuiya hiyo inayowahusisha watu wanaotoka Wilaya za Hanang, Babati, Karatu, Kateshi na Mbulu, ilinzishwa miaka 33 iliyopita ikiwa na lengo la kusaidiana katika masuala ya elimu, afya na njaa.

Tango alisema tangu kuanzishwa jumuiya hiyo, shule 45 katika maeneo mbalimbali ya umoja huo, kufaidika na misaada mbalimbali.

Kadhalika, wilaya nazo zimefaidika na misaada ya majanga ya njaa katika vijiji zaidi ya 25 vilivyopata shida.

"Mambo haya ni sehemu ya kazi za kikundi chetu kusaidia jamii kule tulikotoka pamoja na kwamba kwa sasa hatuishi huko. Tumemwita waziri mkuu mstaafu kuwa mgeni rasmi katika hafla yetu ya leo, kwani ni miongoni mwa wanachama wa Norivada," alisema Tango. Alisema sasa jumuiya hiyo ina wanachama 450 ambao wanashirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Chanzo: mwananchi

Tunaomba Maoni yako Hapa :

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply