» » » WAKAZI WA ARUSHA SASA KULIPIA ANKARA ZA MAJI SAFI NA TAKA KUPITIA M-PESA


Mkuu wa Wilaya ya jiji la arusha, John Mongella,akiongea wakati wa uzinduzi rasmi wa jinsi ya kulipia Ankara ya maji safi kupitia huduma ya M-PESA,kwa wakazi wa mkoa wa jiji la Arusha,kutoka kushoto ni Mwenyekiti kamati ya mawasiliano na ujenzi Zanzibar Bw.Makame Mshimba Mbaruk,Mwenyekiti wa bodi ya (AUWSA) Bw.Felix Mrema.
Arusha, Zaidi ya wananchi 500,000 waishio katika manispaa ya Arusha sasa hawatahitaji tena kupanga foleni ili kulipia ankara za maji. Hii inafuatia ushirikiano baina ya Vodacom Tanzania na mamlaka ya maji safi na maji taka ya Arusha (AUWSA) utakaowezesha malipo hayo kufanyika kupitia huduma ya M-Pesa.

AUWSA ni mamlaka iliyoundwa kisheria chini ya sheria ya utoaji maji kifungu cha 272 ili kuendesha shughuli za upatikanaji wa maji safi na kusimamia maji taka mjini Arusha. AUWSA ilianza kufanya kazi zake kama taasisi huru mwezi Januari, 1998

Huduma ya M-Pesa ina mawakala zaidi ya 40,000 nchi nzima, hivyo kuwezesha urahisi wa malipo ya huduma ya maji kama hii mahala popote pale nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa utoaji huduma hiyo ya malipo, Mkuu wa Wilaya ya jiji la arusha, John Mongella alisema kuwa hatua hii mpya itachangia kwa kiasi kikubwa kuleta huduma bora kwa wakazi wa mji wa Arusha katika viwango vya juu zaidi.

"Hili ni jambo la maana sana ambalo siyo tu kwamba limekuja kwa AUWSA, bali kwa watu wa Arusha kwa ujumla. Ninazishukuru pande zote mbili ambazo zimeshirikiana kufanikisha huduma hii. Nataka kuwahakikishia kuwa serikali imeazimia kuunga mkono juhudi za namna hii za kutumia utaalamu unaolenga kuinua maisha ya wananchi," alisema Mongella.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa AUWSA, Lucy Shushu Koya, alizungumzia jinsi ambavyo kwa kiwango kikubwa wakazi wa Arusha wataepuka usumbufu wa kutumia muda mrefu kwenye foleni za kulipia huduma ya maji na kusema: "Huduma hii ni hatua ya kipekee hasa ikizingatiwa kuwa kuanzia sasa muda ambao mteja angeutumia kusubiri kwenye foleni, badala yake atauingiza katika shughuli nyingine za kila siku kama kazi au biashara. Pia kufanya malipo kupitia M-Pesa kutarahisisha ufanyaji kazi wa mamlaka na kutoa nafasi ya kuongeza ubora wa huduma."

Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini, Philemon Chacha, alisema: "Nawahimiza wakazi wa Arusha watumie huduma ya M-Pesa kulipia ankara za maji kutokana na kuwa ni huduma ya haraka na salama. Hii ni njia ya uhakika ya kuokoa muda malighafi muhimu ya muda, na hivyo ni vyema sote kuitumia."

Ili kufanya malipo kupitia M-Pesa, wateja wanashauriwa kupiga *150*00# kisha kuchagua namba 4, na baada ya hapo kuingiza namba ya biashara (230230). Kufuatia hatua hiyo watatakiwa kuingiza namba ya akaunti na namba ya siri (PIN), halafu watabonyeza 1 kuthibitisha, au 2 kusitisha mhamala.


Mkuu wa Wilaya ya jiji la arusha, John Mongella,wanne toka kushoto akifatilia maelekezo toka kwa Mkuu wa Vodacom kanda ya kaskazini Bw.Philemon Chacha jinsi ya kulipia Ankara ya maji safi kupitia huduma ya M-PESA,mara baada ya kuzindua huduma hiyo mkoani humo ambapo wakazi wa jiji la arusha watakuwa wakilipia Ankara za maji safi na maji taka kwa kupitia huduma hiyo,wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Mwenyekiti kamati ya mawasiliano na ujenzi Zanzibar Bw.Makame Mshimba Mbaruk,Mwenyekiti wa bodi ya (AUWSA) Bw.Felix Mrema naMkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja wa (AUWSA) Masoud Katiba.

Kuhusu Vodacom Tanzania:

Kampuni ya Vodacom Tanzania Limited ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo kupitia taasisi yake ya Vodacom Foundation. Vodacom Foundation ina nguzo kuu tatu: Afya, Elimu na Ustawi wa Jamii. Hadi sasa taasisi hiyo imechangia zaidi ya miradi 120 ya kijamii nchini. Aidha, imeshinda tuzo mbalimbali za kitaifa na za kimataifa katika nyanja ya Uwajibikaji wa Mashirika kwa Jamii. Hizi ni pamoja na East African CSR Awards na Diversion and Inclusion Award ambayo hutolewa na kampuni mama ya Vodafone.

Vodacom Tanzania Limited ni kampuni ya simu za mikononi inayoongoza Tanzania inayotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano. Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya Vodacom Group (Pty) Limited, South Afritca, ambayo pia ni kampuni tanzu ya Vodafone Group UK. Vodacom Group (Pty) Limited inamiliki hisa ailimia 65 Vodacom Tanzania na asilimia 35 zilizobaki zinammilikiwa na Mirambo Ltd.

Vodacom Tanzania imetangazwa kuwa Super Brand (Chapa Bora Zaidi) kwa miaka mitatu mfululizo, kutoka 2009 -2011.


Mkuu wa Wilaya ya jiji la arusha, John Mongella,watano kutoka kushoto waliokaa,akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom na wa mamlaka ya maji safi na maji taka ya Arusha (AUWSA) mara baada ya hafla fupi ya uzinduzi wa kulipia Ankara za maji safi na maji kupitia huduma ya Vodacom M-PESA kwa wakazi wa jiji la arusha.

Tunaomba Maoni yako Hapa :

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply