» » Abiria Dar es Salaam wakwama Ubungo Ni Baada ya Madereva Kugoma








HUDUMA za usafiri katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam, jana zilisimama kwa muda kutokana na madereva wa malori kufunga barabara katika kituo cha mizani cha Kibaha tangu juzi usiku.

Hali hiyo ilileta usumbufu mkubwa kwa abiria waliokuwa wasafiri kwenda nje ya jiji, kwani mabasi yalikosa mahali pa kupita na hivyo kulazimika kusitisha safari.

Msongamano huo ulisababishwa na hatua ya madereva wa malori yanayobeba mizigo yenye uzito kuanzia tani 3.5 na kuendelea, kuamua kuegesha magari yao barabarani kupinga kitendo cha serikali kufuta msamaha wa tozo ya asilimia tano ya mizani.(hd)


Akikizungumza kwa niaba ya madereva wenzake wa mabasi, Salimu Kangeta alisema hawako tayari kuwatoa abiria kituoni huku wakijua kuwa watakwenda kuteseka huko mbele.

Kangeta alifafanua kuwa abiria walifika asubuhi kama tiketi zao zilivyokuwa zikiwaelekeza lakini baadhi yao walishindwa kuondoka kutokana na madereva wengi kukataa kuanza safari kwa sababu barabara ilikuwa na msongamano mkubwa wa malori kuanzia Kibamba hadi Kibaha mizani.

Alisema kuwa katika kuhangaika, wako madereva waliojaribu kupitia njia ya Bagamoyo lakini ilishindikana baada ya kuzuiwa na askari kwa madai kuwa kisheria hawaruhusiwi kupita katika barabara hiyo.

"Kuna askari ambaye hatukumfahamu alikuwa akielekeza madereva kupitia njia hiyo kwa madai alikuwa amewasiliana na RTO wa mkoa wa Pwani kuhusu mpango huo.

"Cha kushangaza baadhi ya madereva walizuiwa kupita katika njia hiyo ya Bagamoyo na kutakiwa kurudi barabara ya Morogoro, huu ni usumbufu tu," alisema.

Kwa mujibu wa dereva huyo, hata kama wangeruhusiwa kupita huko bado magari yanayopita mkoa wa Morogoro kwenda mikoa mingine yasingenufaika na utaratibu huo, bali yale ya kwenda mikoa ya kaskazini pekee.

Kangeta alisema madereva hawapaswi kulaumiwa kwa usumbufu walioupata abiria kwani wao sio chanzo bali wa kulaumiwa ni Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na kikosi cha usalama barabarani kwa kushindwa kudhibiti tukio hilo mapema.

Uegeshaji huo wa malori na kufunga barabara ulianza juzi saa 10 jioni kwenye mizani ya Kibaha baada ya wamiliki wa malori kuwa na mkutano wa kupinga tozo ya asilimia tano ya mizani, ambayo ilikuwa imefutwa.

Aidha katika mkutano huo ilielezwa na wamiliki hao kuwa hali hiyo itasababisha kero kubwa sio kwa wenye malori pekee, bali hata kwenye mizani pia.

Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema suala la msongamano huo ni la kiutawala, hivyo wenye kulitolea ufafanunuzi zaidi ni kikosi cha usalaama barabarani.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili baadaye mchana zilisema kuwa mabasi mengi yalianza safari zao mchana saa sita baada kukwama kuondoka asubuhi.

Tunaomba Maoni yako Hapa :

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply