Lazima wote wawe wana hisia za kweli kutoka ndani ya mioyo yao.
Ndoa si jambo la kukurupuka wala kuamua kuingia kwa maana ya kufanya majaribio. Siyo sahihi hata kidogo.
Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza mambo ya msingi ya kuzingatia wakati ukimtaka mwenzi wa maisha yako. Leo tunaingia katika hatua nyingine. Twende tukaone.
Sifa nyingine muhimu ya kumwangalia mwenzi anayefaa kuwa naye kwenye ndoa ni pamoja na yule mwenye mapenzi ya kweli hasa. Mapenzi ya kweli huonekana haraka sana. Penzi la dhati halijifichi.
Hujitokeza hadharani, wakati mwingine bila hiyari.
Mwenye sifa hii ni msikivu (kwa wanaume na wanawake), muelewa na anayetoa kipaumbele kwa mwenzake. Kama anakupenda kwa dhati ni lazima akupe kipaumbele katika mambo yake.
Si msiri na hutoa nafasi kwa mwenzake kutoa mawazo yake katika mambo yanayomhusu. Hatua hii hutokana na namna anavyomuona mwenzake kama sehemu ya maisha yake.
Unaweza kuwa na mpenzi na mkapanga mipango mbalimbali ya baadaye ikiwemo ndoa lakini akawa na kasoro kubwa zilizojificha. Wakati mwingine kasoro hizo unaweza kuziona lakini usijue kama ni kubwa zinazoweza kuwa tatizo kubwa katika maisha yenu ya ndoa.
Mara nyingi kasoro za mwingine zinaweza kufichwa na mapenzi ya dhati yaliyopo ndani ya mtendwa. Mathalani wewe una mpenzi wako, kwa vile ndani yako kuna mapenzi ya dhati, mwenzako anaweza kuwa anakosea tena makosa makubwa, lakini ukajikuta unavumilia, kudharau au kupuuzia!
Zipo dalili nyingi za mpenzi asiyefaa, lakini hapa nakuletea zile za muhimu zaidi.
Katika makosa makubwa kabisa kwenye uhusiano ni pamoja na kusaliti. Kama mwenzi wako anakusaliti na una ushahidi wa kutosha (hasa kama umemfumania) ni dalili mbaya kwenye ndoa.
Mtu wa aina hiyo hafai kabisa kumfikiria kuungana naye katika ndoa.
Aliye sahihi anapaswa kuwa msikivu, mwenye kupima kila kinachotoka kwenye ulimi wake. Kama katika kipindi cha awali tu, anakuwa mkorofi, vipi kwenye ndoa? Fikiri hili kwa makini.
Tabia hii zaidi ipo kwa wanaume. Kosa dogo tu anamwangushia mwenzake kipigo. Kupigana si mapenzi. Kama bado mpo kwenye uchumba tu, kosa dogo kipigo, vipi mkiingia kwenye ndoa? Tafakari jambo hili utaona ni kasoro kubwa sana.
Hata kama unampenda kwa kiwango gani, huyu hafai kabisa kuwa nawe kwenye ndoa.
No comments: