Habari iliyotolewa jana mchana na HABARI-MAELEZO inasema kuwa Serikali imelizuia gazeti la Mwananchi lililofungiwa kuanzia Septemba 27 kuchapishwa mtandaoni hadi pale adhabu itakapokwisha. Aidha kampuni ya New Habari 2006 pia imezuiwa kuchapisha kila siku gazeti la RAI baada ya moja ya magazeti yake kufungiwa.
Hii ni taarifa kamili kwa vyombo vya habari kutoka IDARA YA HABARI –MAELEZO
Kama mnavyofahamu, Serikali imeyafungia magazeti ya Mtanzania na Mwananchi kwa kuzingatia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na kanuni zake za mwaka 1977. Gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa muda wiki mbili kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 na Gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu au siku 90 kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013.
Aidha tunataka umma ufahamu kuwa Serikali haikukurupuka kufungia magazeti hayo. Uamuzi huo ulifanyika baada ya
kufuata taratibu zote za msingi ikiwemo kuwasikiliza wahusika.
Hata hivyo, tumeona gazeti la Mwananchi baada ya kufungiwa limeendelea kuchapishwa kwenye mtandao wa Internet kinyume cha amri iliyotolewa. Kufanya hivyo ni kosa na Serikali tumewaandikia kuacha mara moja la sivyo, Serikali italazimika kuchukua hatua kali zaidi.
Aidha kampuni ya New Habari 2006 baada ya kufungiwa moja ya magazeti yake, imeanza kuchapisha gazeti la ‘Rai’ kila siku tangu tarehe 29 Septemba mwaka 2013 bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti. Hilo nalo ni kosa, Serikali inawataka kuacha mara moja kuchapisha gazeti hilo kila siku na warudie ratiba yao ya kuchapisha mara moja kwa wiki mpaka hapo maamuzi mengine yatakapofanyika.”
Baada ya amri hiyo Mwananchi walitoa taarifa kupitia Facebook:
Tunasikitika kuwaarifu kuwa kutokana na sababu zisizozuilika, tutashindwa kuendelea kuwaletea habari mpya kupitia tovuti yetu (www.mwananchi.co.tz) na mitandao ya kijamii ya Mwananchi kwa wakati wote ambapo uzalishaji wa gazeti la Mwananchi utakuwa umesitishwa.
Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaosababishwa na hali hii na tunatumaini mtaendelea kuwa nasi wakati wa kipindi hiki kigumu cha mpito. Tunatarajia kurejea rasmi hewani na habari moto moto wiki ijayo, Ijumaa, tarehe 11 October.
Tunawakaribisha muendelee kusoma habari zetu za zamani (archives) kwenye tovuti ya Mwananchi na kurasa zetu za Facebook na Twitter ili mzidi kuhabarika.
Pia tunawakaribisha mtembelee tovuti zetu za www.thecitizen.co.tz na www.mwanaspoti.co.tz ambazo zitaendelea kufanya kazi kwa ufanisi, zikiwaletea habari za uhakika na kuaminika kipindi hiki ambapo Mwananchi imefungiwa.
No comments: